Na Ev. Zachary John Bequeker - Mwanza +255 625966236
Watu wengi wamekuwa wakuwa wakijihoji kama kweli mtu
amezaliwa mara ya pili na bado ni mwombaji kwa nini anaingia majaribuni,
kwanini Mungu ana yaruhusu majaribu?
Kujaribiwa ni kupewa mtihani ambao unatakiwa uufanya na
mwamuzi wa mwisho kwamba utapata alama 0
au 100 ni wewe.
Zifuatazo ni sababu za kuachiliwa kwa majaribu kwetu:
1. Kuongeza imani
Kama nilivyosema hapo juu kwamba majaribu
ni mtihani ambao unapewa wewe uufanye na baadaye matokeo huja kama ni kushinda
au kushindwa. Unaposhinda maana yake unakuwa umeongezeka kiimani na hata wakati
mwingine ukikutana na jaribu la namna hiyo haliwezi kukuyumbisha kwa sababu una
kumbukumbu kwamba hapo awali ulipita katika jaribu hilo na ukalishinda. Na hata
ukipita katika jaribu kubwa zaidi ya lile la awali unakuwa na matumaini na
imani kwamba utashinda kama ulivyoshinda katika jina la Yesu.
1 Petro 1:7 “ili kwamba kujaribiwa kwa
imani yenu, ambayo ina thamani kuu kuliko dhahabu ipoteayo, ijapokuwa hiyo
hujaribiwa kwa moto, kuonekane kuwa kwenye sifa na utukufu na heshima, katika
kufunuliwa kwake Yesu Kristo.”
2. Kuimarisha kiroho
Unapopita katika majaribu maana yake
unakuwa unafanya mazoezi ya mwili ambayo kwa wakati huo unaona kama unaumia
lakini baadaye mwili huimarika na kuwa na uwezo wa kunyanyua vitu vizito, kuzuia
vitu fulani au kumzuia adui. Kama ilivyo kwa mtu anayefanya mazoezi ya
kutunisha misuli kwa kunyanyua vyuma vizito, misuli huvunjika na kuwa dhaifu na
baadaye huimarika. Vivyo hivyo hata kwa mtu anayepitia majaribu huwa dhaifu kwa
muda na baadaye huwa imara kiroho yaani kiroho chake hukomaa kiasi kwamba
hakuna kitu chochote ambacho kinaweza kumyumbisha katika imani. Iwe ni ugumu wa
maisha, kukosa mke, kuchelewa kuolewa, kukosa mtoto katika ndoa, kuugua kwa
muda mrefu n.k
Kama misuli inavyokuwa imara baaada ya
mazoezi vivyo hivyo hata imani ya mtu au kiroho cha mtu huwa imara baada ya
majaribu.
Yakobo 1:2-4 “Ndugu zangu, hesabuni ya kuwa
ni furaha tupu, mkiangukia katika majaribu mbalimbali; mkifahamu ya kuwa
kujaribiwa kwa imani yenu huleta saburi.
Saburi
na iwe na kazi kamilifu, mpate kuwa wakamilifu na watimilifu bila kupungukiwa
na neno.”
3. Ili kuwasaidia watu wengine
Wakati mwingine Mungu huyaachilia majaribu
kwetu ili baadaye tuje tuwasaidie watu watakao pita katika majaribu kama
tuliyoyapitia sisi. Mungu hututumia kuwafariji na kuwatia moyo wengine
waliokatika jaribu kama tulilolipitia.
2 Wakorintho 1:3-5 “Na ahimidiwe Mungu,
Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa rehema, Mungu wa faraja yote;
atufarijiye katika dhiki zetu zote ili nasi tupate kuwafariji wale walio katika
dhiki za namna zote, kwa faraja hizo, tunazofarijiwa na Mungu. Kwa kuwa kama
vile mateso ya Kristo yanavyozidi kwetu, vivyo hivyo faraja yetu inazidi kwa
njia ya Kristo.”
Kukwepa kutokuwa na majaribu ni sawa na
kuikwepa fursa ya kuinuliwa na Mungu.
HITIMISHO: Pamoja na faida hizo tatu za
majaribu lakini ni vyema pia tukatambua Mungu hawezi kutujaribu katika mabaya.
Mabaya hayo ni kama wizi, uzinzi, uasherati na mengine yanayo fanana na haya
yote hutokana na shetani kwa tamaa zetu wenyewe wala si Mungu.
Yakobo 1:13-14 “Mtu ajaribiwapo, asiseme, Ninajaribiwa na
Mungu; maana Mungu hawezi kujaribiwa na maovu, wala yeye mwenyewe hamjaribu
mtu. Lakini kila mmoja hujaribiwa na tamaa yake mwenyewe huku akivutwa
na kudanganywa.”
Mithali 27:21 “……….Na mtu hujaribiwa kwa sifa
zake.”
Unataka kuokoka? Tuma ujumbe kwa WhatsApp au sms kwa namba 0625966236 ukianza na neno "NATAKA KUOKOKA"
HII NI INJILI HALISI MINISTRY, KWA MAWASILIANO +255 621 261 295
No comments: