Na Mchungaji Isaya,
Katika dunia ya leo Mungu anaonekana maskini sana, ndio
maana mtu akifanikiwa anaitwa majina ya kila aina; mara jambazi, freemason, mla
rushwa n.k.
Tunapozungumzia mafanikio, hatuongelei magari, majumba, pesa
bali neno mafanikio linatokano na neno kufanikiwa. Hivyo maana ya kufanikiwa ni
kupata kitu kile ambacho kilikuwa ni haja ya moyo wako, kiwe kizuri au kibaya. Mtu
aliyefanikiwa maana yake ni mtu aliyepata kitu alichokuwa akikihitaji au jambo
alilolikusudia. Tunapata mafanikio kwa njia ya kidunia(kibinadamu) pia yapo
mafanikio yatokanayo na Mungu mwenyewe. Mpaka upate kitu cha Mungu mwenyewe
halisi si kitu rahisi rahisi.
Kila mwanadamu ana mahitaji na unapofanikiwa kuna mambo mawili hutokea:-
Jambo la kwanza Moyo
huchangamka, hufurahi: Biblia inasema katika Mithali 17:22 kwamba “Moyo uliochangamka
ni dawa nzuri” Kumbe moyo unapofurahi, furaha ikiingia matatizo madogo
madogo katika mwili yanajifia menyewe.
Jambo la pili mwili hupata nguvu: nguvu haziko mwilini bali ziko
kwenye akili. Kuna wakati mwili unaweza kuwa unaona umechoka kabisa, umelala
ndani unajiona dhaifu lakini mara ukapigiwa simu ukiambiwa kuna kazi mahali
fulani ya pesa nzuri tu, hapohapo akili itakuijia namna ya kufanya na mara utapata
nguvu.Unapofanikiwa unapata nguvu za kuendelea kuamini kuwa Mungu anaweza
kukufanikishia hata kwa hayo mengine na unapata nguvu za kusonga mbele. Unaofurahi
sio mwili bali ni moyo. Ukipata nguo nzuri unavaa mwili lakini moyo ndio
unafurahi. Moyo ukikasirika hata kama umevaa nguo mpya utaona ni kuukuu.
Mithali 13:12 “Kilichotarajiwa
kikikawia kuja, moyo huugua. Bali haja ya mtu ikipatikana, ni mti wa uzima.”
Kuna njia kuu tatu za kufanikiwa katika jambo lolote lile hapa duniani.
Njia ya kwanza ni Elimu: ni muhimu sana watu kuwa na elimu katika
ulimwengu wa leo kwa sababu mambo hayawezi kufanikiwa pasipo maarifa. Elimu inaweza kukutoa sehemu moja hadi
nyingine. Kila jambo linahitaji elimu na elimu si ya shuleni tu bali elimu
hupatikana popote pale ulipo; kwa mfano umemuona dada fulani kafunga kilemba
chake vizuri na wewe unafunga kama yeye, watu wakikuona wanasema ‘mama
fulani leo umetokelezea hatariii, hongera’ kumbe umeigilizia, ulipata
elimu ya kufunga kilemba kutoka kwa dada yule.
Ukisoma Mithali 15:14 inasema “Moyo
wa mwenye ufahamu hutafuta maarifa” kumbe tunapaswa kuyatafuta maarifa ili
tuwe na ufahamu na tuweze kufanikiwa kwa
jambo fulani. Mtu mwenye maarifa ya jambo fulani uwezo wake wa kufanikiwa huwa
ni mkubwa sana. Mithali 24:5 “…mtu
wa maarifa huongeza uwezo;” Elimu
inaweza kukufanya ukaketi kwa wakuu. Danieli
1:3-6 “Mfalme akamwambia Ashpenazi, mkuu wa matowashi wake, awalete
baadhi ya wana wa Israeli, wa uzao wa kifalme, na wa uzao wa kiungwana;
vijana wasio na mawaa, wazuri wa uso, wajuzi wa hekima, werevu kwa sababu ya
maarifa yao, wenye kufahamu elimu, watakaoweza kusimama katika jumba la mfalme;
tena alimwambia awafundishe elimu ya Wakaldayo, na lugha yao.Huyo mfalme
akawaagizia posho ya chakula cha mfalme, na ya divai aliyokunywa, akaagiza
walishwe hivyo muda wa miaka mitatu; ili kwamba hatimaye wasimame mbele ya
mfalme.”
Njia
ya pili ni watu: Mungu anaweza kutumia watu ili kutufanikishia
mambo yetu. Watu wanaweza kukusaidia kwa kukupa hiki au kile ili ufikie malengo
yako. Inaweza ikawa ni kukusomesha, kukupa mtaji, kukutafutia kazi au hiki au
kile.
Njia
ya tatu ni Mkono wa Mungu mwenyewe: mkono wa Mungu unapotaka kutenda
hauchagui wenye elimu au wasio na elimu. Mkono wa Mungu hauhitaji refarii wa
kukupigia debe ili upate kazi au uolewe. Mkono wa Mungu mwenyewe unapotenda
jambo huwa hauchanganywi na kitu chochote. Mungu ni Mungu mwenye wivu hivyo
anapotaka kutenda huwa natenda mwenyewe ili zile sifa na utukufu usiwe wa
kugawana kwa wanadamu na Yeye, Yeye hutaka sifa zote ziwe zake. Mkono wa Mungu
mwenyewe unamtambua na kumtumia mtu yeyote yule bila kujali elimu yake. Petro
na Yohana hawakuwa na elimu kubwa ya darasani lakini walichapa kazi ya Mungu na
ikasonga mbele. Mkono wa Mungu unamtambua na kumtumia yeyeto yule sawa na Mungu
apendavyo. Mungu akimgusa mtu aje kukuoa hautasumbuliwa katika ndoa, fahamu
wanadamu wanakupa mke/mme lakini hawakusaidii kuishi naye bali Mungu anakupa
mke/mme na anakupa akili ya kuishi naye. Mungu akitenda jambo akili ya kibinadamu haitafasri.
Unaweza ukafanikiwa kwa njia ya elimu
au watu lakini njia hizi huwa zina kasoro. Watu wakitusaidia kupata mafanikio
watataka kurudishiwa shukurani na kama hautafanya hivyo tayari ni kosa kwa watu
hao.
Mungu hafanyi kwa sababu umeomba
bali Mungu hufanya kwa sababu unatembea
vizuri na Mungu, kwa sababu unauhusiano mzuri na Mungu.
Kwa Hana na Sarai njia ya elimu na
watu zilishindwa kuwasaidia ili wapate watoto lakini Mkono wa Mungu mwenyewe
uliwagusa wakapata watoto katika jina la Yesu. Tunamwamini Mungu asiyezuiwa na
mazingira, utasa wa Hana haukumzuia Mungu kumpatia Hana mtoto, utasa na ubibi
kizee wa Sara haukumzuia Mungu kumpatia Sara mtoto. Mungu akitaka kufanya jambo
hazuiwi na kitu chochote.
Tufanye nini ili tuuone mkono wa Mungu mwenyewe maishani mwetu?
Jambo
la kwanza, jifunze kumtanguliza Mungu katika mambo yako yote unayotaka
kuyafanya au unayoyafanya. Ukimtanguliza Mungu utakuwa tayari kumsikia anasema
nini juu ya unachokifanya kama kwa Petro na Yohana; Petro na Yohana
walimtanguliza Mungu ndio maana hata walipotishiwa kukamatwa hawakutanguliza
sababu zao binafi kwamba ‘oooh sasa ona tunaenda kufungwa’ Matendo
ya Mitume 4:19 “Petro na Yohana wakawajibu wakawaambia,
Kwamba ni haki mbele za Mungu kuwasikiliza ninyi kuliko Mungu, hukumuni ninyi
wenyewe” Mtangulize Mungu wala si
wanadamu, wanadamu inafikia mahali wanachoka kukusaidia lakini Mungu hachoki. Usiwe
kama Esau aliyetanguliza njaa akauza uzaliwa wake wa kwanza. Mathayo 6:33 “Bali
utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa.”
Jambo
la pili, kubali kuanza na mambo madogo: kubali
kuanza mambo madogo yaliyo manyonge, dhaifu na baadaye Mungu atakuinua. Mungu
huanza na watu waliochini kabisa wasiojua chochote na hao ndio huwatumia na
baadaye huwainua na kuwapandisha juu. Je, unataka kitu kikubwa? Kubali kuanzia
chini. Iwe ni kazi kubali kuanza na kazi hata ya chini kabisa na baadaye utaona
unainuka; iwe ni biashara usitamani hadi uanze na mtaji mkuuuubwa, hapana! Anza
na mtaji wako wa kawaida tu na Mungu atakuinua taratibu utayafikia mafanikio
yako.
Jambo
la tatu, kubali kuwa mvumilivu:Mungu hatubariki kwa sababu tunataka
tubarikiwe bali Mungu hutubariki kwa sababu ni muda muafaka wa kubarikiwa. Unamkuta binti analalamika “yaani kwa kweli
muda unaenda hata siolewi, angalia matiti yanaanza kuning’inia” binti
nakushauri vumilia tu,hayo matiti yataning’inia lakini hayawezi kudondoka, kuna watu
wanapenda matiti makubwa kama ya kwako.
Wakati mwingine usitamani mafanikio ya
mwenzako kwa sababu hujui siri ya mafanikio yake.
HII NI INJILI HALISI MINISTRY, KWA MAWASILIANO +255 621 261 295
No comments: