» » NITOEJE ILI NIBARIKIWE KWA KUTOA KWANGU?

NI UTOAJI UPI WENYE BARAKA?


Na Ev. Zachary John Bequeker
Watu wamekuwa wakihoji kwamba ni njia ipi sahihi ya utoaji? Jibu ni kwamba njia za utoaji ziko nyingi sana. Kuna kujitoa kwa mali zako , fedha zako, nguvu zako, au akili yako pia kwa kutoa mawazo sahihi ili kufanikisha jambo fulani. Lakini katika haya yote na mengine leo tuzungumzie hasa utoaji wa mali, fedha na nguvu.
Kutoa mali au vitu tulivyonavyo: Yesu alipokuwa akiingia Yerusalemu alikuwa amempanda mwanapunda, mwanapunda huyo alikuwa si wa Yesu bali alikuwa ametolewa na mtu mmoja ili Yesu ampande, huo ni mfano wa kutoa vitu au mali. Wengine waliotoa vitu ni Habili(Wanyama), Kaini(mazao), Sulemani, Ibrahimu na wengine weeengi ambao tukisema tuwataje basi tutajaza ukurasa huu.
Kutoa fedha:Tunatoa fedha kama sadaka kanisani, pia tunatoa fedha kwa wahitaji. Tunatoa ili kuwafadhili wengine waweze kufanikisha jambo jema. Katika ibada za Yesu mwenyewe kulikuwa na utaratibu wa utoaji na Yuda ndiye alikuwa mtunza fedha .
Kujitoa kwa nguvu au muda wetu: katika kujitoa kwa nguvu ni pale mfano kanisani kuna kazi fulani unaenda kushiriki kuifanya au unawasaidia watu fulani kufanya jambo fulani lililojema.hapa mara nyingi mtu hutumia maarifa yake aliyonayo na ujuzi wake ili kufanikisha kazi ile.
Mchango wa mawazo:.Hii ni namna nyingine ya utoaji lakini ikiwa ni hatua ya awali isiyo na ufanikishaji. Kwanini? Ni kweli kwamba jambo lolote haliwezi kufanyika kwa usahihi pasipo mawazo sahihi. jambo lolote haliwezi kufanyika kwa ufanisi pasipo maarifa. Lakini pia mawazo hayo hayawezi kutekelezeka pasipo kuwepo na watu wa kujitoa mali zao, fedha zao, nguvu zao na muda wao ili kufanikisha jambo lile. Hivyo basi mchango wa mawazo ni mzuri lakini usiache kutea na vingine kwa kusema “mimi nilichangia mawazo yangu kwa hiyo nimemaliza.”
Utoaji huu wote huweza kutolewa kwa mtu muhitaji au taasisi yoyote yenye uhitaji kwa lengo la kuvitumia katika mambo mema; taasisi hiyo inaweza kuwa ni kanisa, shule, hospitali n.k
Kuna watu wanatabia ya kutoa halafu baadaye huanza kulalamika, kimsingi watu hawa hawakutoa kwa moyo bali walitoa ili kumridhisha mtu fulani au kwa kujionesha kwa watu fulani. Mungu hafurahii watu wanaotoa si kwa moyo.
Usifanye jambo lolote kwa kulazimishwa wala kunung’unika , usitoe chochote kwa manung’uniko wala malalamiko, vivyo hivyo usitoe chochote ambacho unajua baadaye utamsema mtu yule na kumnyanyasa kwa vile ulivyompa badala yake toa au fanya lolote kwa furaha bila manung’uniko.
Anayebarikiwa ni yule anayetoa kwa moyo wala si kwa kulazimishwa. Kuna watu wengine utoaji wao mpaka walazimishwe na kuna watu wengine huwalazimisha wengine kutoa vitu vilivyo nje ya uwezo wao, kufanya hivi ni hakumfurahishi Mungu na wala Mungu hawezi kumbariki mtu wa jinsii hii.
Kutoa ni moyo. Mtu hawezi kutoa kama hajaguswa moyoni mwake atoe pia mtu akitoa kwa kuklazimishwa bila kuguswa moyoni mwake Mungu hawezi kumbariki.(Kumbukumbu la Torati 15:10-11)
Si tu kwamba Mungu hupendezwa na wanaotoa kwa moyo bali huwabariki pia.
Tupende kushiriki mema tuliyonayo pamoja na wengine wenye uhitaji huku tukikumbuka kwamba tunapowapa watu vitu nasi Mungu hutupa na kuzidi (Luka 6:38, Mithali 22:9).
Tunapotoa kwa manung’uniko na kulalamika tunakuwa tunamzuia Mungu kutubariki.
Mungu asili yake ni utoaji, kwanza kabisa alianza kutoa mudawake, nguvu zake na maarifa yake ili kuumba Mbingu, dunia na vyote viujazavyo. Pili, akaitoa pumzi yake kwa Adamu aliyekuwa udongo akawa mtu hai. Tatu,akatoa mavazi kwa Adamu na Hawa walipokuwa uchi bustanini. Nne, hakuishia hapo, akamtoa mwanawe wa pekee Yesu Kristo ili afe kwa ajili ya dhambi zetu(Yohana 3:16).
Kumbuka kila kilichochema hushuka kutoka kwa Mungu. Yeye anaitwa ‘YEHOVAH JILEH’ yaani Mungu mpaji anayeshughulika na mahitaji yetu. Mungu ndiye mwenye vitu vyote na ameahidi kumbariki kila atoaye. Kumbe tunapotoa tunakuwa tunamrudishia sehemu kidogo tu ya vitu alivyotupa.
Utoaji wa mwanamke mjane: Katika utoaji wa mwanamke mjane wa Marko 12:41-44 tunajifunza mambo matatu. Moja, Mungu hutuangalia tunapokuwa tunatoa. Pili, Mungu haangalii ni kiasi gani umetowa bali kitu ulichotoa kina thamani kiasi gani kwako. Tatu, Mungu anamtaka kila mmoja atoe hata kama ni maskini,. Usiache kutoa kwa kisingizio wewe ni maskini ukitoa elfu moja watakucheka wale waliotoa laki moja au zaidi. Wewe toa ulichonacho na Mungu atapendezwa nawe kama alivyotoa yule mwanamke mjane(maskini).
Hitimisho:anyayebarikiwa ni yule anayetoa kwa moyo wala si kwa kulazimishwa(2 Wakorintho 9:7) kama walivyofanya watakatifu waliotutangulia( 2 Wakorintho 8:1-5).Toa kwa moyo lakini fahamu kuwa APANDAYE HABA, ATAVUNA HABA (2 Wakorintho 9:6) panda kwa UKARIMU ILI UVUNE KWA UKARIMU. Kwa hiyo wewe toa unachotoa ukijua kipimo unachopimia wengine ndicho utakachopimiwa.
Je, unataka kubarikiwa zaidi? Toa kwa moyo
Je, unataka kubarikiwa zaidi? Toa zaidi.
Ukweli wa Biblia
1 Wakorintho 16:2 “Siku ya kwanza ya juma kila mtu kwenu na aweke akiba kwake, kwa kadiri ya kufanikiwa kwake; ili kwamba michango isifanyike hapo nitakapokuja;”
2 Wakorintho 8:1-5 “1 Tena ndugu zetu, twawaarifu habari ya neema ya Mungu, waliyopewa makanisa ya Makedonia; 2 maana walipokuwa wakijaribiwa kwa dhiki nyingi, wingi wa furaha yao na umaskini wao uliokuwa mwingi uliwaongezea utajiri wa ukarimu wao.3 Maana nawashuhudia kwamba, kwa uwezo wao, na zaidi ya uwezo wao, kwa hiari yao wenyewe walitoa vitu vyao; 4 wakituomba sana pamoja na kutusihi kwa habari ya neema hii, na shirika hili la kuwahudumia watakatifu.5 Tena walitenda hivi si kama tulivyotumaini tu, bali kwanza walijitoa nafsi zao kwa Bwana; na kwetu pia, kwa mapenzi ya Mungu. 6 Hata tukamwonya Tito kuwatimilizia neema hii kwenu kama vile yeye alivyotangulia kuianzisha.”
2 Wakorintho 9:6-8 “6 Lakini nasema neno hili, Apandaye haba atavuna haba; apandaye kwa ukarimu atavuna kwa ukarimu. 7 Kila mtu na atende kama alivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni, wala si kwa lazima; maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu. 8 Na Mungu aweza kuwajaza kila neema kwa wingi, ili ninyi, mkiwa na riziki za kila namna siku zote, mpate kuzidi sana katika kila tendo jema;”
Matendo ya Mitume 20:35 “Katika mambo yote nimewaonyesha ya kuwa kwa kushika kazi hivi imewapasa kuwasaidia wanyonge, na kuyakumbuka maneno ya Bwana Yesu, jinsi alivyosema mwenyewe, Ni heri kutoa kuliko kupokea.”
Mithali 11:24-25 “24 Kuna atawanyaye, lakini huongezewa zaidi; Kuna azuiaye isivyo haki, lakini huelekea uhitaji. 25 Nafsi ya mtu mkarimu itawandishwa; Anyweshaye atanyweshwa mwenyewe.”
Yakobo 1:17 “Kila kutoa kuliko kwema, na kila kitolewacho kilicho kamili, hutoka juu, hushuka kwa Baba wa mianga; kwake hakuna kubadilika, wala kivuli cha kugeuka-geuka.”
Luka 6:38 “Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwa-sukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa.”
Mithali 22:9 “Mwenye jicho la ukarimu atabarikiwa; Maana huwapa maskini chakula chake.”
Marko 12:41-44 “41 Naye akaketi kulielekea sanduku la hazina, akatazama jinsi mkutano watiavyo mapesa katika sanduku. Matajiri wengi wakatia mengi.42 Akaja mwanamke mmoja, mjane, maskini, akatia senti mbili, kiasi cha nusu pesa. 43 Akawaita wanafunzi wake, akawaambia, Amin, nawaambia, Huyu mjane maskini ametia zaidi kuliko wote wanaotia katika sanduku la hazina; 44 maana hao wote walitia baadhi ya mali iliyowazidi; bali huyu katika umaskini wake ametia vyote alivyokuwa navyo, ndiyo riziki yake yote pia.”
...............................
Je, unataka kuokoka?
Tuma neno "NATAKA KUOKOKA" kwa SMS au WhatsApp kwa +255625966236
Facebook Group: Injili Halisi Ministry
KWA MAFUNDISHO TEMBELEA;
🔗zakachekainjili.blogspot.com
💕 Sharing is Caring💓

Pakua App Ya Injili Halisi -Bofya Hapa Flower
HII NI INJILI HALISI MINISTRY, KWA MAWASILIANO +255 621 261 295

About INJILI HALISI MINISTRY

Zachary, most known as Zakacheka is the founder of the Injili Halisi Ministry. He is a member of Full Gospel Bible Fellowship Church.. He lives in Mwanza,Tanzania. 0621261295.
«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments:

Leave a Reply