Na Ev. Zachary
John Bequeker (+255625966236)
Kumdharau mtu ni
tabia ya kutomthamini, kutomheshimu
na kumpuuza.
MITHALI 14:21 “Amdharauye
mwenzake afanya dhambi; Bali amhurumiaye maskini ana heri.”
Katika
andiko hili limejipambanua waziwazi kwamba dharau ni dhambi.
Kwa nini dharau ni dhambi?
Dharau ni
dhambi kwa sababu neno la Mungu limetuagiza tupendane katika Yohana 15:12 “Amri yangu ndiyo hii, Mpendane, kama nilivyowapenda ninyi.” Si rahisi kumpenda mtu usiyemheshimu.
Kumbe palipo dharau hakuna upendo.
Kama mtu
humpendi huwezi kuumia juu yake.Mungu kwa kuupenda ulimwengu wa dhambi akawa
tayari kumtoa mwanae wa pekee Yesu Kristo, na si hivyo tu bali pia Yesu Kristo
kwa upendo wake akawa tayari kujitoa ili afe kwa ajili ya dhambi zetu. Yesu
alitutanguliza kwanza sisi akatuona kuwa ni wa thamani kwake hivyo hatupaswi
tuangamie. Kumbe na sisi tukipendana, tutaheshimiana na kila mmoja
atamtanguliza mwenzie. Tujifunze kuwaona wengine kuwa ni bora kuliko sisi.
WARUMI 12:10 “Kwa pendo la udugu, mpendane ninyi kwa ninyi; kwa heshima
mkiwatanguliza wenzenu”
Kuna watu
tumekuwa tukijiona kuwa ni bora kuliko wengine kazini, kanisani, katika
familia, ukoo au taifa pia. Kujiona kuwa ni bora kuliko wengine ni kujihesabia
haki. Mungu humshusha mtu anayejiona kuwa ni bora kuliko wengine, tena
huwashusha hata kuzimu(motoni) kwa sababu dharau ni dambi.
Neno
linasema katika 1 Wathesalonike 5:14 kwamba
“…. watieni moyo walio dhaifu; watieni
nguvu wanyonge; vumilieni na watu wote.” Tunapaswa kuwatia moyo wale
tunaoona ni dhaifu, duni wala hawawezi kuliko kuwasema na kuwadharau bure.
Tunapaswa
kuchukuliana na walio dhaifu. Mfano ni kazini, kanisani au katika familia
usifikiri wote mtakuwa na uwezo sawa katika utendaji, wewe utakuwa bora katika
hiki lakini pia hata hao unao waona kuwa ni dhaifu watakuwa ni hodari katika
jambo fulani ambalo wewe huliwezi; usiwadharau, watie moyo yaani watie nguvu
kwa wanachokifanya na uwape mbinu mbadala ili wafanye vyema zaidi kuliko
kuwasema tu. Kumbuka kila mmoja hutenda jambo kwa uwezo wake aliojaliwa(1 PETRO 4:11).
Hebu
tuchukuliane na wale walio dhaifu wala tusitake wafanye kama tulivyo sisi. Ni
vyema kutamani watu wengine wawe katika viwango ulivyonavyo vya utendaji au vya
kiroho lakini kumbuka kwamba kila mmoja amejaliwa kwa namna yake. Ndio maana
Paulo mtume wakati mmoja alitamani watu wasioe na kuolewa lakini hakulazimisha
baada ya kutambua kuwa kuna wachache waliojaliwa wala si wote. Hivyo kumbe basi
katika kazi, kanisa, familia au uongozi tusitegemee kuona wote tukiwa tunatenda
kwa namna moja, huyu atakuwa hivi na yule vile.
Neno la
Mungu linatuhimiza tuchukuliane wala tusidharauliane. Kuna watu wamekuwa
wakiwadharau watumishi wa Mungu wa Mbinguni aliye hai na kujiona kuwa wao ni
bora, wengine mmekuwa mkiona kuwa dhehebu lenu ndio bora kuliko mengine na kwa
namna hiyo mmekuwa ni watu wa mipasho tu badala ya kumhubiri Kristo kama
isemavyo 1 Wakorintho 1:23-24
mmekuwa ni watu wa kuyahubiri madhehebu yenu, mmekuwa ni watu wa kuhubiri
mitazamo yenu wala si neno la Mungu. Ndugu zangu tusidharauliyane tukijua
kwamba kwa maneno yetu tutahukumiwa (MATHAYO
12:37). Kumbuka yule mtumishi kipindi anapata maono ya kuanzisha huduma
wewe hukuwepo na hata kama ulikuwepo huwezi fahamu vyema anayeujua ukweli ni
mwanzilishi wa huduma wengine tutabaki kupiga kelele bure.
WAFILIPI 2:3-5 “Msitende
neno lo lote kwa kushindana wala kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu, kila mtu
na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake.4 Kila mtu asiangalie mambo
yake mwenyewe, bali kila mtu aangalie mambo ya wengine.5 Iweni na nia iyo hiyo
ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu”
WAGALATIA 6:1-5 “1
Ndugu zangu, mtu akighafilika katika kosa lo lote, ninyi mlio wa Roho mrejezeni
upya mtu kama huyo kwa roho ya upole, ukijiangalia nafsi yako usije ukajaribiwa
wewe mwenyewe.2 Mchukuliane mizigo na kuitimiza hivyo sheria ya Kristo.3 Maana
mtu akijiona kuwa ni kitu, naye si kitu, ajidanganya nafsi yake. 4 Lakini kila
mtu na aipime kazi yake mwenyewe, ndipo atakapokuwa na sababu ya kujisifu ndani
ya nafsi yake tu, wala si kwa mwenzake. 5 Maana kila mtu atalichukua furushi
lake mwenyewe.”
Siri ya kuinuliwa
na Mungu ni kukubali kujishusha nakujitoa kwa ajili ya hao na kwa jinsi hii
Mungu atapendezwa nasi (MATHAYO
22:25-28) .
Tujifunze
namna ya kuwasaidia hao tunaowaona kuwa ni dhaifu ili wawe hodari na kwa jinsi
hii tutang’aa (DANIELI 12:3).
Usimdharau
ndugu yako, mfanyakazi menzako, kiongozi mwenzio wa dini, mshirika mwenzio
kanisani, jirani yako au yeyote yule kumbuka hana apendaye awe dhaifu.
Usidharau dhehebu fulani au watu wa dhehebu fulani. Ukiona wako kinyume na
utaratibu unapaswa kufanya mambo
yafuatayo; moja waombee, pili sema nao wala hupaswi kujipiga kifua na kujidai,
Mungu atakuhesabu kuwa wewe ni mpumbavu. Wewe unayejiona ni tajiri usiwadharau
maskini na pia wafundishe watoto wako wawaheshimu watoto wa maskini na kuwaona
nao ni binadamu kama wao.
LUKA 18:9-14 “9
Akawaambia mfano huu watu waliojikinai ya kuwa wao ni wenye haki, wakiwadharau
wengine wote… Yule Farisayo akasimama akiomba hivi moyoni mwake; Ee Mungu,
nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu wengine, wanyang'anyi, wadhalimu, wazinzi,
wala kama huyu mtoza ushuru. 12 Mimi nafunga mara mbili kwa juma; hutoa zaka
katika mapato yangu yote.13 Lakini yule mtoza ushuru alisimama mbali, wala
hakuthubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali alijipiga-piga kifua akisema,
Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi.14 Nawaambia, huyu alishuka kwenda
nyumbani kwake amehesabiwa haki kuliko yule; kwa maana kila ajikwezaye
atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa.”
INJILI HALISI MINISTRY
(Online Ministry)
+255
625966236/ +255 758590489 / +255 67590489
HII NI INJILI HALISI MINISTRY, KWA MAWASILIANO +255 621 261 295
No comments: