Na Mwinjilisti Zachary John Bequeker
+255625966236/+255758590489
Yesu akiwa amempanda punda kuingia katika mji wa Yerusalemu
umati mkubwa wa watu walikusanyika wakatandaza matawi yao ya mitende na mavazi yao njiani, wakimpatia heshima ya
Kifalme. Mamia ya watu walipaza sauti zao wakisema " Hosana, Mwana wa Daudi;
ndiye mbarikiwa, yeye ajaye kwa jina la Bwana; Hosana juu mbinguni."
MATHAYO 21:1-11 – Yesu aliingia Yerusalemu kama
Mfalme.
“1 Hata
walipokaribia Yerusalemu, na kufika Bethfage, katika mlima wa Mizeituni, ndipo
Yesu alipotuma wanafunzi wawili akiwaambia,2 Enendeni mpaka kijiji kile
kinachowakabili, na mara mtaona punda amefungwa, na mwana-punda pamoja naye;
wafungueni mniletee…..7 wakamleta yule punda na mwana-punda, wakaweka nguo zao
juu yao, naye akaketi juu yake. 8 Watu wengi katika ule mkutano wakatandaza
nguo zao njiani; na wengine wakakata matawi ya miti, wakayatandaza njiani.9 Na
makutano waliotangulia, na wale waliofuata, wakapaza sauti, wakisema, Hosana, Mwana wa Daudi; ndiye mbarikiwa,
yeye ajaye kwa jina la Bwana; Hosana juu mbinguni. 10 Hata alipoingia
Yerusalemu, mji wote ukataharuki, watu wakisema, Ni nani huyu?11 Makutano
wakasema, Huyu ni yule nabii, Yesu, wa Nazareti ya Galilaya.”
Jumapili ya mitende ndio mwanzo wa wiki takatifu ambayo ni
siku maalumu ambayo Yesu alianza safari
yake kuelekea msalabani.
Neno la Mungu linatuambia watu walikata matawi ya mitende na
kuyapunga hewani na mengine wakayatanda chini naye Yesu akapita juu yake
akiingia katika mji wa Yerusalemu.Matawi ya mitende yanawakilisha mema na
ushindi na ilikuwa ni alama yaa ushindi mkubwa juu ya kifo.
1 WAKORINTHO 15:55 “Ku wapi, Ewe mauti, kushinda
kwako? U wapi, Ewe mauti, uchungu wako?”
Yesu alichagua kupanda punda ambacho ni kitu kilichotimiza
unabii wa Agano la Kale katika ZEKARIA
9:9. Katika kipindi cha biblia ilikuwa wafalme wakilakiwa wakiwa wamepanda
punda. Punda huwakilisha amani, kwa hiyo wale waliomlaki walionesha kujawa na
amani. Yesu anatajwa kuwa ni Mfalme wa amani.
ZEKARIA 9:9 “ Furahi sana, Ee binti Sayuni; Piga kelele, Ee
binti Yerusalemu; Tazama, mfalme wako anakuja kwako; Ni mwenye haki, naye ana
wokovu; Ni mnyenyekevu, amepanda punda, Naam, mwana-punda, mtoto wa punda.”
Watu walipiga kelele wakisema “Hosana! Ndiye mbarikiwa ajaye
kwa jina la Bwana” walimtambua Kristo kuwa ni Mfalme. Neno “Hosana” linamaanisha “Okoa sasa”. Walisema “Hosana”
wakitambua yeye ndiye mwokozi ambaye muda si mrefu anaenda kuwapatia wokovu.
YOHANA 12:12-15 “12 Nayo siku ya pili yake watu wengi walioijia
sikukuu walisikia ya kwamba Yesu anakuja Yerusalemu; 13 wakatwaa matawi ya
mitende, wakatoka nje kwenda kumlaki, wakapiga makelele, Hosana! Ndiye
mbarikiwa ajaye kwa jina la Bwana, Mfalme wa Israeli! 14 Naye Yesu alikuwa
amepata mwana-punda, akampanda, kama vile iliyoandikwa, 15 Usiogope, binti
Sayuni; tazama, Mfalme wako anakuja, amepanda mwana-punda.”
ZABURI 118:25-26 “25 Ee Bwana, utuokoe,
twakusihi; Ee Bwana, utufanikishe, twakusihi. 26 Na abarikiwe yeye ajaye kwa
jina la Bwana; Tumewabarikia toka nyumbani mwa Bwana.”
WARUMI 10:9 “9 Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa
kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua
katika wafu, utaokoka.”
Biblia inasema kwamba “Yesu aliulilia mji”. Kipindi
wanaendelea kushangialia Yesu alitambua moyoni mwake kuwa muda si mrefu ujao
hao wanaomshangilia watamgeuka, watamsaliti na kumuua. Moyo wake ulihuzunika na kuona jinsi
walivyokuwa wakimhitaji Mwokozi.
LUKA 19:41-42 “41
Alipofika karibu aliuona mji, akaulilia, 42 akisema, Laiti ungalijua, hata wewe
katika siku hii, yapasayo amani! Lakini sasa yamefichwa machoni pako.”
Jumapili ya Matawi inatukumbusha kuwa Kristo ni mkuu kuliko
mtu yeyote yule. Katika dunia ya le wanadamu hutafuta mtu wa kupigana naye ili
wapate ushindi lakini yesu kwa upendo wake akawa tayari kupigana kwa ajili ya
ulimwengu wote na akatupatia ushindi mkuu kupitia kifo chake. Na hii ndio
sababu kuu ya kusheherekea juma hili. Kwa sababu ya Sadaka ya Kristo pale
msalabani tumewekwa huru kutoka katika mauti, yaani mauti ya milele na kuwekwa
katika uzima wa milele.
YOHANA 11:25 “25 Yesu akamwambia, Mimi ndimi
huo ufufuo, na uzima. Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi”
Tunapaswa kufurahi sana katika kipindi cha juma hili.
Adui analijua hilo na unaweza
kukisia kuwa katika juma hili hawezi kuupata ushindi kamwe.
Katika juma hili takatifu, namwomba Mungu mawazo yetu kuwaza
juu ya Kristo aliye Mfalme wetu.
Tuelekeze akili zetu katika kumwabudu Bwana wetu, kumshukuru
kwa zawadi njema ya sadaka yake, kusheherekea nguvu ya ufufuo, na maisha mapya
tunayoyapata kwake.
2 WAKORINTHO 9:15 “15 Mungu ashukuriwe kwa sababu
ya kipawa chake, tusichoweza kukisifu kama ipasavyo.”
BONYEZA HAPA KUUNGANA NASI FACEBOOK: INJILI HALISI
HII NI INJILI HALISI MINISTRY, KWA MAWASILIANO +255 621 261 295
No comments: