» » SOMO: KUWAOGOPA WANADAMU HULETA MTEGO


MITHALI 29:25 "Kuwaogopa wanadamu huleta mtego; Bali amtumainiye Bwana atakuwa salama"

Mtu anayeogopa anakuwa na hofu ndani yake. Hofu hiyo inampelekea kushindwa kufanya yaliyo mapenzi ya Mungu na kufanya kama wanavyotaka watu fulani ili aepukane na madhara ambayo yangetokea kwake endapo angetenda tofauti na kudhani kwamba kufanya hivyo ndivyo atakuwa salama Kumbe sivyo.
Mtu anayeogopa wanadamu anaweza kusema uongo, kuzini, kufanya uasherati, kuua, kumkana Yesu, kuacha wokovu, kuwaongoza wengine upotevuni, kumkosoa Mungu juu ya uumbaji. Sasa tuangalie jambo moja baada ya jingine:-

1. UONGO
Ibrahimu kwa kuogopa kuuawa akasema uongo kuwa Sara si Mke wake bali ni dada yake MWANZO 12:11-20"Ikawa alipokuwa karibu kuingia Misri, akamwambia Sarai mkewe, Tazama, najua ya kuwa u mwanamke mzuri wa uso; basi itakuwa, Wamisri watakapokuona watasema, Huyu ni mkewe; kisha wataniua mimi na wewe watakuacha hai. Tafadhali useme, wewe u ndugu yangu, iwe heri kwangu kwa ajili yako, na nafsi yangu iishi kwa ajili yako.....Ndipo Farao akamwita Abramu, akasema, N'nini hili ulilonitendea? Mbona hukuniambia ya kuwa huyo ni mkeo?, Mbona ulisema, Huyo ni umbu langu, hata nikamtwaa kuwa mke wangu? Basi sasa, huyo mke wako umchukue, uende zako." Pia soma MWANZO 20:1-11

Isaka naye alisema uongo kama wa baba yake Ibrahim kwa kuogopa kuuliwa na kunyang'anywa mke MWANZO 26:6-11 "Watu wa mahali hapo wakamwuliza habari za mkewe. Akasema, Ni ndugu yangu huyu maana aliogopa kusema, Ni mke wangu, watu wa nchi wasije wakamwua kwa ajili ya Rebeka; kwa maana alikuwa mzuri wa uso."

Tunapokuwa wakweli tunajiepusha na uovu. MITHALI 16:6 "Kwa rehema na kweli uovu husafishwa; Kwa kumcha Bwana watu hujiepusha na maovu." Kumbe tunaepukana na uovu kwa kusema kweli japo kwa muda huo tutaona kama tunaumizwa au kuteswa kwa kusema ukweli.

Vilevile kwa kuwaogopa wanadamu watu wamekuwa wakisema uongo hata katika makanisa ili wapate msaada kwa kuogopa kuitwa na watu kuwa 'wameishiwa, maskini,' na hata kuogopa kupambana na njaa.

Amri ya tisa inatuzuia kushuhudia uongo kwa maana uongo ni dhambi (KUTOKA 20:16) na waongo wote watapata hukumu sawa sawa na UFUNUO WA YOHANA 21:8 "Bali waoga, na wasioamini, na wachukizao, na wauaji, na wazinzi, na wachawi, na hao waabuduo sanamu, na waongo wote, sehemu yao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti. Hii ndiyo mauti ya pili."

2. UZINZI NA UASHERATI
Watu kwa kuogopa kuitwa hanisi au wasion na nguvu za kiume wameangukia katika dhambi ya uzinzi na uasherati. katika KUTOKA 14:20 amri ya Mungu inasema "Usizini". Pia wazinzi mahali pao ni Jehanam(UFUNUO WA YOHANA 21:8)

Kijana hapaswi kufanya mapenzi (tendo la ndoa kabla ya kutoa au kuolewa) kufanya hivyo ni dhambi. WAEFESO 5:3 "Lakini uasherati usitajwe kwenu kamwe, wala uchafu wo wote wa kutamani, kama iwastahilivyo watakatifu"

3: UUAJI
Mfalme Daudi kwa kuogopa kuwepo kwa mtu aliyemchukulia mme yaani hakutaka kabisa kumuona kwani ingekuwa ni fedheha kwake kuwa alichukua mke wa mtu.

Herode na yeye kwa kuogopa kuambiwa ukweli  kuwa hakufanya vyema kumchukua mke wa nduguye akamkamata Yohana Mbatizaji na akamuua MATHAYO 14:1-12.

Tunapoambiwa ukweli tusichukie na hata kutaka kuwaua hao wanaotuambiwa ukweli Kumbe kinyume chake tunapaswa tuwapende.

4. KUMKANA YESU
Petro alimkana Yesu kwa sababu aliogopa kupigwa na watu (YOHANA 18:17,26-27).

5. KUACHA WOKOVU NA KURUDI DHAMBINI

Dema alikuwa ni mtumishi mzuri sana aliyetenda kazi pamoja na Mtume Paulo kwa viwango vya juu sana  lakini kwa sababu ya kuogopa kuonekana mshamba akaupenda ulimwengu yaani matendo ya giza akaiacha imani.
FILIMONI 1:24 "na Marko, na Aristarko, na Dema, na Luka, watendao kazi pamoja nami."

2 TIMOTHEO 4:10 "Maana Dema aliniacha, akiupenda ulimwengu huu wa sasa..."

Hizi ni nyakati za mwisho neno la Mungu linatuhimiza tushike sana tulichonacho ambao ndio wokovu tulioupokea kwa Neema.
 UFUNUO WA YOHANA 3:11 "Naja upesi. Shika sana ulicho nacho, asije mtu akaitwaa taji yako."

6. KUWAONGOZA WATU UPOTEVUNI

Haruna kwa kuwaogopa wana wa Israeli akachonga ndama ili waiabudu. KUTOKA 32:1-6 "Hata watu walipoona ya kuwa Musa amekawia kushuka katika mlima, wakakusanyana wakamwendea Haruni, wakamwambia, Haya! Katufanyizie miungu itakayokwenda mbele yetu, kwa maana Musa huyo aliyetutoa katika nchi ya Misri hatujui yaliyompata. Haruni akawaambia, Zivunjeni pete za dhahabu zilizo katika masikio ya wake zenu, na wana wenu, na binti zenu, mkaniletee.....Akaipokea mikononi mwao akaitengeneza kwa patasi, akaifanya iwe sanamu ya ndama kwa kuiyeyusha; nao wakasema, Hiyo ndiyo miungu yako, Ee Israeli, iliyokutoa katika nchi ya Misri."


Vivyo hivyo hata sasa wachungaji wengi kwa kuogopa kukimbiwa na waumini wamekuwa wakihubiri kama jinsi waumini wanavyotaka na si kama jinsi Roho Mtakatifu anavyotaka kusema na wana wa Mungu.Kwa kuwa watu wamekuwa wakihitaji maneno laini ya kufariji, hadithi na vichekesho Wachungaji nao wamekuwa wakifuata matakwa yao. ISAYA 30:9-10 "Kwa maana watu hawa ni watu waasi, watoto wasemao uongo, watoto wasiotaka kuisikia sheria ya Bwana; wawaambiao waonaji, Msione; na manabii, Msitoe unabii wa mambo ya haki, tuambieni maneno laini, hubirini maneno yadanganyayo;"

WARUMI 16:18 "Kwa sababu walio hivyo hawamtumikii Bwana wetu Kristo, bali matumbo yao wenyewe; na kwa maneno laini na ya kujipendekeza waidanganya mioyo ya watu wanyofu.". 
Mtu aliyeokoka  mahali hapa si salama kwake kwani mwisho ni kupotea.
YEREMIA 50:6 "Watu wangu wamekuwa kondoo waliopotea, wachungaji wao wamewapoteza; wamewapotosha milimani; wamekwenda toka mlima hata kilima, wamesahau mahali pao pa kupumzika." 

Neno la Mungu linatuhimiza tutoke kati yao mara moja  2 WAKORINTHO 6:17 "Kwa hiyo, Tokeni kati yao, Mkatengwe nao, asema Bwana, Msiguse kitu kilicho kichafu, Nami nitawakaribisha"

Ndugu yangu usikae mahali    unaona wao kila kitu ni sahihi, kunywa pombe, kuvuta sigara , madawa ya kulevya, uzinzi, uasherati, masengenyo, uongo, mizaha, fitina na mengine yanayofanana na hayo na wanasema mtu ukiokoka unafanya lolote tu au unavaa vyovyote tu na haina shida, hakika hapo si mahali salama ndugu yangu.

7. KUMKOSOA MUNGU
Watu kwa kuogopa maneno ya kuitwa 'SURA MBAYA', 'SURA MNG'O' wanaanza kujichubua. Wengine hawana hips kubwa wanaweka za bandia, wengine matiti ya bandia na wengine wanatafuta  wawe na matako ya WOWOWO hivyo wanameza vidonge, wanachomwa sindano na wengine wanapakaa dawa. Wengine hadi wanatamani kubadili jinsia. Wengine wanadiliki kubadili matumizi yasiyo ya mwili na kuyafanya yawe, mfano Usoga na usagaji.Je, Mungu aliyekuumba hivyo tumboni mwa mama yako hakuona vyema ? Kwa nini kumuudhi Mungu kwa kuogopa kuchekwa na wanadamu? Kwani hapa utaishi milele? Baada ya maisha mafupi ya hapa duniani utakufa, jiulize ukifa utakuwa wapi?.    Je, Mungu aliyeweka sehemu za siri za mwanamke na Mwanamme hakujua matumizi yake? Kwanini wewe Mwanamme unamtaka Mwanamme? Kwanini wewe mwanamke unamtaka mwanamke? Kwanini wewe mwanamke huridhiki na sehemu rasmi ya tendo la ndoa hadi unahitaji na sehemu za haja kubwa?  Kwa nini wewe mwanamke huridhiki hadi ulazimishe kufanyiwa na sehemu za haja kubwa  na tena akikataa mmeo unamtishia kumuacha, kwanini?  

Wengine manywele bandia ya wafu , katani na plastiki jamani kwanini usijikubali jinsi ulivyo? Kama umeshindwa kujikubali wewe kama wewe utamkubali nani? Hebu badilika katika Jina la Yesu, sema Amen.

8. KUABUDU SANAMU
Watu kwa kuogopa kutengwa na dini, ndugu, jamaa, marafiki na hata wafanya kazi wenzao wameona bora waendelee kukaa mahali wanapoabudu sanamu kwa kuogopa kwamba watakosa wa kuwazika jamani! Hivi maiti tangu lini ikakosa wa kuizika? Nani anaweza kukaa na maiti ndani? Je, ni nani hata kama ni jirani anweza kuiona maiti nje akaiacha? Hakuna hata mmoja. Hebu tuache uwoga. Neno la Mungu linatukataza kuabudu sanamu tunapaswa tutii na si vinginevyo.

KUTOKA 20:3-5 "Usiwe na miungu mingine ila mimi. Usijifanyie sanamu ya kuchonga, wala mfano wa kitu cho chote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia. Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi, Bwana, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu; nawapatiliza wana maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao," 

Wengine kwa kuogopa kutengwa na ukoo wamejikuta wakijihusisha na matambiko ya kiukoo. Kufanya hivyo ni kuabudu sanamu yaani miungu.
Pia soma YOHANA 9:22;12:42

9: KUISHI MAISHA YA UNAFIKI
Watu wamekuwa wakiishi maisha ya unafiki kwa kuwaogopa wanadamu. Ndugu yangu unatafuta kumpendeza nani Mungu au wanadamu?

10. KUISHI MAISHA YA KUAZIMA
Kwanini nasema maisha ya kuazima? Kitu chochote cha kuazima hakimfanyi mtu kuishi kwa furaha ya muda mrefu kwani ni cha muda na italazimika kukirudisha. Ndivyo ilivyo watu wengi kwa kuogopa kuitwa wasio na kazi. Mtu hana kazi lakini akiamka asubuhi tu machomeko na tai jamani! Machomeko na tai huna kazi ili nini? Tafuta kazi chakalika na Mungu atakuinua. Mungu hambariki kamwe mtu mvivu asiyefanya kazi. Mungu huwabariki watu kupitia kazi za mikono yao.

Ni mimi Ev. Zachary John Bequeker
+255 (0)625 966 236
+255 (0)758 590 489

Pakua App Ya Injili Halisi -Bofya Hapa Flower
HII NI INJILI HALISI MINISTRY, KWA MAWASILIANO +255 621 261 295

About INJILI HALISI MINISTRY

Zachary, most known as Zakacheka is the founder of the Injili Halisi Ministry. He is a member of Full Gospel Bible Fellowship Church.. He lives in Mwanza,Tanzania. 0621261295.
«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments:

Leave a Reply