» » MAANA YA NENO UBATIZO


Na Mwinjilisti Zachary John Bequeker

Neno "UBATIZO" linatokana na neno la Kiyunani "βαπτιζω" ambalo herufi zake zinasomeka "BAPTIDZO". Neno hili halimaanishi kunyunyuzia (sprinkle) au kumwagia (pour). Neno hili linamaanisha Kuzamisha (to dip) au kutumbukiza (to immerse). Kumbe basi, neno " BAPTIDZO" lina maanisha " UBATIZO WA MAJI MENGI AU MAJI TELE" ambapo mtu huzamishwa mwili wote.

»Yesu alibatizwa ubatizo wa maji tele , kwa kulithibitisha hilo tunaona katika MATHAYO 3:16 "Naye Yesu alipokwisha kubatizwa mara akapanda kutoka majini; na tazama, mbingu zikamfunukia, akamwona Roho wa Mungu akishuka kama hua, akija juu yake;"

» Mitume nao waliwabatiza watu kwa maji mengi. MATENDO YA MITUME 8:36-39. "Wakawa wakiendelea njiani, wakafika mahali penye maji; yule towashi akasema, Tazama, maji haya; ni nini kinachonizuia nisibatizwe?.......wakatelemka wote wawili majini, Filipo na yule towashi; naye akambatiza. Kisha walipopanda Kutoka majini..."

»Yohana alikuwa akibatiza hata baada ya Yesu kuanza huduma, alikuwa akibatiza katika maji tele YOHANA 3:22-23 " Baada ya hayo Yesu na wanafunzi wake walikwenda mpaka nchi ya Uyahudi; akashinda huko pamoja nao, akabatiza. Yohana naye alikuwa akibatiza huko Ainoni, karibu na Salimu, kwa sababu huko kulikuwa na maji tele; na watu wakamwendea, wakabatizwa."

JE, ILI TUOKOKE NI LAZIMA TUBATIZWE?
»Tunapokea wokovu kwa kukiri kwa vinywa vyetu (WARUMI 10:9-10).

»Kwa mujibu wa Neno la Mungu, Ubatizo siyo jambo linalohitajika ili mtu apate wokovu.

»Hatupati wokovu kwa matendo ya mwili bali tunaupokea wokovu kwa Neema kwa njia ya Imani (MATENDO YA MITUME 15:11; WARUMI 4:1-25; WAGALATIA 2:16; WAEFESO 2:8-9; WAFILIPI 3:9).

»Kama UBATIZO wa maji ulihitajika ili watu waokoke(wapate wokovu), tungetarajia mahali pote ilipohubiriwa injili watu wangebatizwa. Paulo hakubatiza popote katika kuhubiri kwake. Tunaona katika 1 WAKORINTHO 15:1-4 "......na kwa hiyo mnaokolewa; ikiwa mnayashika sana maneno niliyowahubiri isipokuwa mliamini bure..........". Katika 1 WAKORINTHO 1:17 Paulo anasema "Kristo hakunituma ili nibatize bali nihubiri Habari Njema". Andika hili liko wazi kabisa kuonyesha tofauti ya UBATIZO na WOKOVU. Kama ni lazima mtu abatizwe ndipo aokoke ingekuwa vipi Paulo kuhubiri Injili na si Ubatizo? Hakuna ambaye angeokoka.

»Injili ni uweza wa Mungu uletao Wokovu.

MFANO WA WATU WALIOPOKEA WOKOVU BILA KUBATIZWA

1: Mwanamke Kahaba
»Yesu alimwambia mwanamke kahaba katika LUKA 7:37-50 "..... Umesamehewa dhambi zako......imani yako imekuokoa"

2: Mwanamke aliyepooza
»Yesu alimwambia yule mwanamke aliyepooza katika MATHAYO 9:2 "Jipe moyo mkuu mwanangu, umesamehewa dhambi zako".

3: Mtoza Ushuru
»Yesu alitoa mfano wa mtoza ushuru kuwa alisamehewa dhambi kwa kukiri kwa kinywa chake na si kwa kubatizwa (LUKA 18:13-14).

4: Muovu msalabani

»Yesu alimwambia muovu msalabani " Leo hivi utakuwa pamoja nami peponi (paradiso)". Hapo hakuna ubatizo wa maji uliofanyika  (LUKA 23:39-43).

»Mifano hii yote inathibitisha kuwa msamaha wa dhambi ni tofauti na UBATIZO wa maji. Kwa msingi huo basi, hatuna kumbukumbu ya mitume kubatizwa badala yake Yesu anasema  katika YOHANA 15:3 " Mmekwisha kuwa safi kwa sababu ya lile neno nililowaambia"  na katika LUKA 10:20 Anasema wafurahi kwa kuwa majina yao yameandikwa mbinguni.

»Kuna maandiko mawili yanachanganya watu kwa jinsi UBATIZO na WOKOVU unapotajwa pamoja. Katika MATENDO YA MITUME 2:38 Inasema "Tubuni mkabatizwe...... mpate ondoleo la dhambi" Inamaanisha kwamba ubatizo wa maji hauhitajiki ili mtu aokoke bali ni hatua ya pili ya nje baada ya hatua ya kwanza ya kutubu dhambi. Hii ni hatua ya pili ya nje (kimwili) baada ya hatua ya kiroho.

Pia katika MARKO 16:16 "Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini atahukumiwa" Pia hapo tunaona asiye amini ndiye atakaye hukumiwa na si asiyebatizwa. Pia hapa napo ubatizo unatajwa kama hatua inayofuata baada ya kuamini kiroho.

MAMBO MATATU YAHUSUYO UBATIZO
»Ubatizo hutupatia mambo matatu Kutokana na WARUMI 6:1-10 "Hamfahamu ya kuwa sisi sote tuliobatizwa katika Kristo Yesu tulibatizwa katika mauti yake?
..Basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake, kusudi kama Kristo alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzima.Kwa maana kama mlivyounganika naye katika mfano wa mauti yake, kadhalika mtaunganika kwa mfano wa kufufuka kwake..."

1: Ubatizo ni ishara ya kufa, kuzikwa na kufufuka kwa Kristo.

»Tunaposimama katika maji tunawakilisha Yesu msalabani.

»Tunapozamishwa katika maji tunaonyesha kuzikwa kwa Kristo.

»Tunapoibuka kutoka ndani ya maji tunaonyesha kufufuka kwa Kristo.

2: Ubatizo ni Ushuhuda kwetu kuwa tumeoshwa dhambi zetu.

»Tunapozamishwa ndani ya maji tunakubali dhambi zetu zinaoshwa na tunapoibuka tunakuwa tumefufuliwa kuishi maisha mapya katika Kristo.

3: Ubatizo ni uthibitisho wa kuwa sisi ni Wakristo (WARUMI 6:3-4)

»Kunyunyuziwa au kumwagiwa maji kichwani ulipokuwa mtoto mchanga(baby) au kipindi ulipokuwa mdogo huwezi kupambanua mema na mabaya hakuna maana, Ubatizo huo hauna sifa zote tatu zilizotajwa hapo juu.

Litaendelea..........
Na Mwinjilisti Zachary John Bequeker
INJILI HALISI MINISTRY
+2556259666236/+255758590489/+255673590489
EMAIL: zacharybequeker@gmail.com

Pakua App Ya Injili Halisi -Bofya Hapa Flower
HII NI INJILI HALISI MINISTRY, KWA MAWASILIANO +255 621 261 295

About INJILI HALISI MINISTRY

Zachary, most known as Zakacheka is the founder of the Injili Halisi Ministry. He is a member of Full Gospel Bible Fellowship Church.. He lives in Mwanza,Tanzania. 0621261295.
«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments:

Leave a Reply