Shetani huwaijia watu waliookoka kama Malaika wa nuru akitaka kuwageuza na kurudi tena dhambini.
Tunapookoka na kuamua kumfuata Yesu tunayabadili maisha yetu na kuyageuza kabisa na kuishi kama Bwana apendavyo. Hivyo basi Shetani naye hufanya juu chini, kila namna ili kuona anatugeuza tena kurudia yale yale tuliyoyaacha na kutuondoa kuwa wana wa Mungu sawa sawa na YOHANA 1:12 na kutufanya kuwa watoto wake shetani sawa sawa na 1 YOHANA 3:8-10 "atendaye dhambi ni wa Ibilisi; kwa kuwa Ibilisi hutenda dhambi tangu mwanzo. Kwa kusudi hili Mwana wa Mungu alidhihirishwa, ili azivunje kazi za Ibilisi. Kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, kwa sababu uzao wake wakaa ndani yake; wala hawezi kutenda dhambi kwa sababu amezaliwa kutokana na Mungu."
Ni lazima tuzijue mbinu anazotumia Shetani kuwageuza watu, kwani pasipo kuzifahamu mbinu zake tutajikuta tukigeuzwa na kurudi kuyatenda yale tuliyoyaacha awali. Unapozifahamu mbinu za adui yako unakuwa na asilimia nyingi za kuweza kumpiga (2 WAKORINTHO 2:11). Shetani hutuijia akitaka kutugeuza kwa njia ambayo hatutaweza kugundua kuwa ni Shetani na kuona kama ni mtu atuhurumiaye. 2 WAKORINTHO 11:14-15 "Wala si ajabu. Maana Shetani mwenyewe hujigeuza awe mfano wa malaika wa nuru. Basi si neno kubwa watumishi wake nao wakijigeuza wawe mfano wa watumishi wa haki, ambao mwisho wao utakuwa sawasawa na kazi zao.". Shetani hutumia hata watu tunaowajua kuwa ni watumishi wa Mungu, ndugu, jamaa, marafiki wakionekana kana kwamba wanatuhurumia kumbe la! bali wanataka kutupoteza. Kimsingi si wao bali ni Shetani anayetenda kazi ndani yao.
Shetani haogopi kiwango cha kiroho cha mtu. Kwani humwijia mtu kulingana na kiwango chake cha kiroho kama ni kiwango cha chini huijiwa kwa kiwango cha chini na hata kama ni mtu mwenye viwango vya juu kiroho huijiwa kwa viwango vya juu pia. Aliyemgeuza HAWA ndiye aliyemgeuza MKEWE AYUBU, ndiye aliyemgeuza MKEWE LUTU na ndiye aliyemgeuza DEMA, YUDA ISKARIOTE, HARUNI, WANAISRAELI na wengine wengi katika biblià . Kama tunavyoona kwa HAWA katika MWANZO 3;1-3 hivyo hivyo hata kwetu huja kwa kitu kile kile tukiaminicho na kuona kama tukifanya tutapata faida kubwa sana kumba la! mwisho wake ni majuto na kugeuzwa. Tunatakiwa kuwa makini sana na mtu ambaye tunaona ana maneno ya kutugeuza kutenda yale neno la Mungu linatukataza hatupaswi kabisa kumsikiliza bila kujali ni nani hata kama ni Mchungaji, Nabii, au Mtume yeyote yule kwani Hawa makosa aliyoyafanya ni kumsikiliza Shetani aliyekuwa ndani ya nyoka. Katika WAEFESO 4:7 tunaambiwa "wala msimpe Ibilisi nafasi." Kumbe hatupaswi kuwapa nafasi ya kuzungumza nasi watu ambao tunaona mazungumzo yao yana lengo la kubomoa yale mema tuliyoyajenga.
Tusiseme kuwa sisi tuna muda mrefu katika wokovu na kuona kuwa Shetani hatuwezi bali tuwe na tahadhari wakati wote kwani 1 WAKORINTHO 10:8-12 inasema Basi mambo hayo yaliwapata wao kwa jinsi ya mifano, yakaandikwa ili kutuonya sisi, tuliofikiliwa na miisho ya zamani. Kwa hiyo anayejidhania kuwa amesimama na aangalie asianguke.'
Tusisikilize watu walioshindwa kwani hao hutaka nasi tuwe kama wao. Hutaka watugeuze na kuwa kama wao walivyo ili tufanane kama Shetani alivyofukuzwa mbinguni hakupenda kuona Adamu na Hawa wakistarehe katika bustani ya Edeni ndiposa alipofanya juu chini ili nao wafukuzwe katika bustani hiyo.
Dema aliacha wokovu kwa sababu hakuzifahamu fikra za shetani (2 TIMOTHEO 4:10).
Uzinzi na Uasherati unaweza kutugeuza kama Samsoni (WAAMUZI 16:1-2,15-21). Uhusiano wa boyfriend na girlfriend hutuondoa katika wokovu hivyo tusishiriki kabisa. 1 WAKORINTHO 10:8 "Wala msifanye uasherati, kama wengine wao walivyofanya, wakaanguka siku moja watu ishirini na tatu elfu".
2 TIMOTHEO 2:22 "Lakini zikimbie tamaa za ujanani; ukafuate haki, na imani, na upendo, na amani, pamoja na wale wamwitao Bwana kwa moyo safi."
WAEFESO 5:3 "Lakini uasherati usitajwe kwenu kamwe, wala uchafu wo wote wa kutamani, kama iwastahilivyo watakatifu;"
Mungu hataki kuona uasherati ukiwako kwetu. Ili kuwa salama ni lazima kuzijua fikira za yule adui Shetani kwani wengi amewageuza na kumfuata yeye kwa kutozifahamu mbinu zake.
Vilevile Shetani hutumia Pesa kutugeuza kama YUDA (LUKA 22:3-6)
Pesa ina nguvu ya kumgeuza mtu.
1 TIMOTHEO 6:10 "Maana shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana na Imani, na kujichoma kwa maumivu mengi."
Pia tunapaswa kuwa mbali na watu wanaopingana na kweli (neno la Mungu) kwani neno la Mungu lina sema katika 1 WAKORINTHO 15:33 "Msidanganyike; Mazungumzo mabaya huharibu tabia njema." Kwa hiyo unapokuwa unasikiliza maneno ya watu wanaoipinga kweli ya neno la Mungu fahamu kwamba kuna hatari kubwa ya kugeuzwa na kuwafuata hao. Usiwafuate wao bali mfuate Yesu ambaye anaitwa neno tena ndiye njia yaani njia ya Uzima.
YOHANA 14:6 "Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi."
Natumaini uko tayari kuokoka, sasa fuatisha maneno haya. Sema " Bwana Yesu nimejigundua kuwa mimi ni mwenye dhambi . Nakuomba unisamehe Bwana. Futa jina langu katika vitabu vya hukumu na uliandike katika kitabu cha uzima wa milele. Nipe uwezo wa kuyashinda majaribu ya ulimwengu huu wa sasa na uniwezeshe kulipenda neno lako na kuliishi bila kubagua katika Jina la Yesu...Amen!"
Sasa tayari umeokoka jambo la kuzingatia tafuta kanisa linalohubiri kweli ya neno la Mungu bila kupindisha pindisha. Kwa msaada, maombi/maombezi na ushauri wasiliana nami WhatsApp kwa Simu namba +255-625-966-236 pia nifuate facebook kwa jina la Zachary John Bequeker.
Ni mimi Mwinjilisti Zachary John Bequeker
INJILI HALISI MINISTRY
+255-625-966-236
+255-758-590-489
+255-673-590-489
❤ *Sharing is Caring*
```Kuna baraka nyingi sana kwa kila atakaye share ujumbe huu```
www.zakachekainjili.blogspot.com
MUNGU AKUBARIKI❗
HII NI INJILI HALISI MINISTRY, KWA MAWASILIANO +255 621 261 295
No comments: